Advertisement

Responsive Advertisement

KUSHINDWA ILI KUFANIKIWA: SIMULIZI YA BRAINBONGO

Katika mitandao ya kijamii napendelea zaidi Twitter nikihitaji kujifunza na kupanua upeo wangu japo pia hutumia muda mwingi sana Instagram kutangaza kazi zangu, kuburudika na kutafuta inspiration. Katika kurasa ninazozifuata katika mtandao wa Twitter, ipo moja ambayo huwa ninaitembelea zaidi inayomilikiwa na kaka yangu Balozi wa Tanzania nchini Korea ya Kusini Togolani Mavura @tonytogolani. Niliwahi kukutana naye mara kadhaa mwaka 2015 nikiwa katika majukumu yangu ya upigaji picha. Wakati huo sikumjua ni nani, na nilikua sijaanza kumfuatilia ila ninatumaini kujifunza zaidi siku nyingine nikipata fursa ya kukutanana naye.


Tweets zake ni darasa huru la maisha lililosheheni mafunzo, busara na hekima mtambuka. Hapo nyuma mara kwa mara alikua akalichangamsha darasa kwa nasaha za washahuri wake mbalimbali. Watu wengi mimi nikiwa mmoja wao tulifurahishwa sana na nasaha kutoka kwa mshauri wake wa mambo ya anasa na starehe. 

Katika maktaba ya tweets zake kuna moja ilinigusa kwa namna ya kipekee zaidi na ilisema, “Tunaamka kuhangaika tena sababu bado tuna chembe ya tumaini kuwa leo yaweza kuwa bora kushinda jana na hata tusipofanikiwa leo, pengine tutafanikiwa kesho. Katika maisha, poteza vyote lakini usipoteze matumaini. Ukipoteza matumaini, umepoteza sababu ya kuishi.” Ilinigusa kipekee kwa sababu katika maisha yangu kwa nyakati mbili tofauti binafsi nilihisi kupoteza matumaini na hata kufikiria ni afadhali kufa kuliko kuwa hai. Ni imani yangu hali hii ni hadithi ya watu wengi na leo nimeamua kuisimulia nyakati mojawapo na pengine hadithi yangu inaweza kumpa mtu mmoja sababu ya kutopoteza matumaini.


Mara ya kwanza nimehisi kupoteza matumaini ni siku niliyopokea matokeo yangu ya kidato cha sita yaliyovunja moyo wangu. Nilipata Division 0 katika mchepuo wa fizikia, kemia na hisabati mwaka 2014. Ni hadithi ndefu yenye visa na mikasa hasa ukizingatia kwamba nilipata Division 1 katika mtihani wa kidato cha nne. Mungu akinijalia nitapata nafasi ya kuisimulia siku moja ila leo naomba nikusimulie kuhusu matumaini. Baada ya kupata taarifa hiyo nilisikia uzito wa dunia yote umenielemea, nililia kwa uchungu kuliko nilivyowahi kulia hapo awali. Nilitamani dunia ipasuke niingie ili niikwepe hatma yangu. Niliwaza namna taarifa hiyo itakavyomvunja moyo baba yangu Mzee Boniphace Chacha ambaye amenilea na kunisomesha mimi na ndugu zangu katika mazingira magumu. Nakumbuka siku moja mwanzoni mwa mwaka 2008 akiwa ananipeleka kujiunga na kidato cha kwanza Morogoro Lutheran Junior Seminary alinisihi nijitahidi kusoma kwa bidii na yeye atajitahidi kunisomesha hata kama atalazimika kuvaa bukta badala ya suruali ili kusave hela zaidi ili tusikose ada. Niliwaza walezi wangu ambao kwa hakika walipigwa na bumbuwazi kutokana na namna walivyokua wananifahamu, kunipenda na hata kuniamini. Niliwaza nitaificha wapi aibu yangu mbele ya walimu walionifundisha na hata wakati mwingine kuwekeza muda wao wa ziada ili tuweze kufaulu. Nilijiuliza ni vipi nitawakabili rafiki zangu tuliosoma na kukua pamoja ukizingatia kwamba nilizoeleka kuwa mwanafunzi anayefaulu vizuri na mara kwa mara kuwa katika nafasi za uongozi. Binafsi pia, nilikua nakabiliana na msongo mkubwa wa mawazo maana waswahili wanasema uchungu wa msiba aujuaye mfiwa. Nilihisi kukata tamaa ya kuendelea kuishi, ila Mungu akaniokoa.


Baada ya kulia na machozi kuisha nilipiga moyo konde na kumuomba Mungu anionyeshe njia. Nilimwambia niko tayari kuendelea kupambana nikamuomba anionyeshe namna. Akanikumbusha kuwa kila mtu ni wa kipekee na ana sababu ya kuwa hapa duniani. Hakuna mwenye akili yako, hakuna mwenye mwili wako, hakuna mweye maono yako, hakuna mwenye kipaji chako na kutokuendelea kuishi kabla ya muda uliopangiwa na Mungu mwenyewe ni kuidhulumu dunia mawazo yako. Ni sawa na kulikimbia jukumu. Usipofanya wewe nani atafanya? Je, hata akifanya mwingine anaweza kufanya kama wewe? Jibu nililoanza kupata lilinipa tumaini. Tumaini la kuendelea kupambania sehemu yangu katika dunia. Niliamua kuanza tena. Kuanza na yale ambayo nilikua nayajua, yale yaliyokua yananinyima usingizi na kunipa sababu ya kuamka kila siku. Hapo nyuma nilitazama filamu moja ya kimarekani na kuna mahali muigizaji kinara anasema ,"When you do not know what to do, do what you know”. Katika maisha pamoja na kutafuta ni jambo la muhimu kutosahau kuishi, kufanya yale yanayokusisimua na kukupa furaha. Hii balance ndio fuel ya matumaini. Pengine namna nyingine ya kupata tumaini ni kuangalia watu/vitu unavyojivunia na kufanya matendo yanayougusa moyo wako na/au mioyo ya wengine.


Mwenyezi Mungu ametuumba kila mtu kwa kusudi lake na ndani ya kila mmoja wetu kaweka tayari kila unachokihitaji kuliishi hilo kusudi. Ukipata nafasi soma andiko lililopita KILA MTU NI MAHIRI KWENYE ENEO LAKE LA KUJIDAI ila kupata ufahamu zaidi juu ya kusudi la Mungu kwako na namna ya kulitambua. Ziko ingredients nyingi zinazoweza kukusaidia ufanikiwe katika kusudi lako ila ingredients zote ambazo ni za muhimu zaidi (core ingredients), zinazokutofautisha na wengine ziko ndani yako, hazitoki nje (sio external factors). Nafikiri ni sahihi pia kusema kwamba Mungu ameuweka uwezo wa kupambana na kila changamoto itakayokuja mbele yako katika safari ya kulitimiza hilo kusudi, kila mmoja wetu kwa kadri ya ukubwa wa jukumu lake. Watu wengi wanafikia hatua ya kupoteza matumaini pale ambapo sababu yao ya kuishi  inapokua matatani au kushindwa kwa kiwango kikubwa (catastrophic fail). Kushindwa kunaweza kuleta maumivu, fedheha na hata kukata tamaa. Ila ukweli ni kwamba bila kushindwa hatuwezi kukua. Matatizo yapo ili kutukomaza zaidi na kupima kiwango cha imani na utayari wetu kupambania kile tunachokitafuta. Kwa maneno mengine kushindwa ni kiungo muhimu katika mafanikio kama ilivyo gravity ili kitu chochote kiweze kupaa.  Ndege inaweza kupaa na kubakia angani kwa sababu ya uwezo wa kutengeneza nguvu zaidi (lift) kuishinda nguvu hiyo ya mvutano kutoka chini (kani mvutano au gravity).

Msongo wa mawazo uliokithiri ama sonona (depression) ni tatizo kubwa sana katika jamii yetu. Tatizo ni kubwa zaidi kwa wanaume/vijana wa kiume ambao kwa asili tunategemewa kuwa jasiri, kujikaza, kupambana na hata ikibidi 'kufa kiume'. Msanii Dizasta Vina alisema, "uanaume sio cheo, uanaume ni jukumu" na unaposhindwa kutimiza majukumu huweza kuleta mawazo ambayo yasipodhibitiwa yanaweza kusababisha sonona na hata hisia za kukata tamaa ya kuishi. Ukiwa katika hali hii nakushauri utafute msaada badala ya kufa kiume. Kuomba msaada unaposhindwa ni ishara ya nguvu si udhaifu. Zungumza na mtu unayemwamini, atakaye kusikiliza bila kukuhukumu au mtu mwenye busara, hekima na mwenye kukutakia mema. Pia unaweza kuchukua wasaa peke yako kumuomba Mungu wako ili akuelekeze namna unavyoweza kuibadilisha changamoto yako kuwa fursa ya ukuaji. Jambo baya zaidi kukutokea linaweza kuwa jambo jema zaidi kuwahi kukutokea ila huwezi kujua kama utakata tamaa. Kwa wale wapenzi wa kusoma, kuna self-help books nyingi zinazoweza kukusaidia kupata mtazamo mbadala. Jambo la msingi usipoteze matumaini, kama bado unaweza kupumua, unaweza kuendelea kupambana. Usipoteze matumaini, tafuta sababu ya kuendelea kuishi.


Maisha ni safari na kila unachopitia siku hadi siku bila kujali ni kibaya au kizuri ndio maisha yenyewe. Kinachowatofautisha watu wanaofanikiwa na wanaoshindwa ni mtazamo na haswa pale unaposhindwa au kukutana na changamoto. Japokuwa nilishindwa mtihani wa shuleni, sikukubali kuamini kuwa ndio kushindwa pia mtihani wa maisha. Mwaka 2012 nikiwa kidato cha 5 niliasisi wazo ambalo baadaye tarehe 4 Septemba 2014 lilizaa kampuni ya ubunifu iitwayo BRAINBONGO kwa kushirikiana na marafiki zangu wachache niliofahamia nao hapo shuleni na kugundua uwezo wao wa kipekee. Tumekuwa tukishirikiana kwa takribani miaka 10 sasa na BrainBongo imekua daraja la kila mmoja wetu kuishi ndoto zake. Nafikiri ni sahihi kusema bila kukutana na hawa vijana wabunifu na kushirikiana BrainBongo isingekuwepo leo. Nafikiri pia kushindwa ule mtihani kulinifanya kuzipambania ndoto zangu kwa nguvu na akili zangu zote kwa kuwa sikua na kitu cha ku-fall back on mambo yalipokua/yanapokua magumu. Nina shabaha moja tu, kufuata na kuziishi ndoto zangu na kuwasaidia vijana wenzangu kufikia ndoto zao. Ni kati ya maamuzi ninayojivunia sana kuyafanya katika maisha yangu. Sina majuto kwa sababu niliamua kumwamini Mungu, kuamini maono aliyonipatia na kuwaamini wenzangu. Muda ndio msema kweli. Nakukaribisha kuungana nasi katika hii safari yetu ya matumaini. Let's re-define the African consciousness and re-discover what is possible in Africa!

Kufahamu zaidi kuhusu BRAINBONGO na shughuli tunazofanya angalia tovuti yetu www.brainbongo.co.tz


Post a Comment

1 Comments

  1. Thanks for the story hope it gonna be someone’s survival guide..keep it up man 🤗

    ReplyDelete

If you like this post be sure to leave a comment and share it with your friends. It will make my day!