Nilipokua shule ya msingi tulifundishwa maana ya methali HUJAFA, HUJAUMBIKA ni kwamba mwili wa binadamu unaweza kubadilika kimaumbile wakati wowote angali wakati akiwa hai. Hivyo basi haifai kwa sababu yoyote ile kumcheka, kumdhihaki au kumkejeli mtu ambaye ana ulemavu wa kiungo mwilini mwake. Aliyekufa ndo amekamilika, safari yake imefika mwisho. Binafsi nakubaliana na hii fikra kwa asilimia mia moja lakini sio muumini wa dhana ambayo elimu yetu imetuaminisha kuwa kuna namna moja tu ya kufikiri na hiyo pekee ndio sahihi. Ukiwa na fikra tofauti umekosea, unastahili kufeli. Leo naomba nikosee maana nina fikra tofauti juu ya maana ya methali hii. Ungana nami...
Watu wengi hupewa sifa na heshima wanazostahili wakishakufa. Wakati wa uhai wao watu huwachukulia "poa", hawautambui au kuuthamini mchango wao mpaka wakishakufa na pengo lao kuonekana. Watu wachache sana katika historia walifanikiwa "kuumbika" angali wakiwa hai. Kwa haraka na kwa uchache watu wanaokuja kichwani ni kama Nelson Mandela, Michael Jackson, Steven Hawkings, Muhammad Ali na wengineo. Wapo pia wenye bahati zaidi ambao wanapewa tuzo za heshima sana au kupendwa na mamilioni ya watu angali wakiwa hai kama Barak Obama, Pele, Beyonce, Dalai Lama, Dr Salim Ahmed Salim, Abdulrazak Gurnah na wengineo.
Binafsi, walikuwepo watu watatu (3) ambao japokua sikuwafahamu kiundani ila vifo vyao viliniumiza sana kama walikuwa ni watu wangu wa karibu. Kwa bahati nzuri niligundua uwezo wao mkubwa kifikra na hata kuweza kushawishiwa na maisha yao.
Mwaka 2012 nilipata bahati ya kushiriki maazimisho ya kumbukumbu ya kifo chake wilayani Butiama, mkoani Mara ambapo nilijifunza zaidi kuhusu maisha yake. Nilifurahi kujifunza kuwa pia alikua msomaji mzuri wa vitabu na nilipata nafasi ya kutembelea maktaba yake. Kwa wasiofahamu, Mwl Nyerere alikua akichunga mifugo ya baba yake na akiwa na umri wa miaka 12 alilazimika kutembea takriban kilomita 35 ili kufika shule aliyokua akisoma, shule ya msingi ya Mwisenge iliyoko Musoma Mjini. Niaamini kuwa uzoefu alioupata toka akiwa mdogo mpaka alipokua Waziri mkuu na baadaye Rais ulimpa mtazamo mpana zaidi juu ya maisha na mahitaji ya kila mwananchi wake bila kujali vipato au hali zao kimaisha. Maisha yake ni deni kubwa kwangu na nafikiri linapaswa kuwa deni kwa vijana wengi wa kitanzania. Swali kubwa kwetu ni kwa namna gani tunaweza kuitumikia Tanzania yetu ambayo nilisoma mahali kuwa akiwa katika nyakati za mwisho wa uhai wake alituusia kuipenda "kama tunavyowapenda mama zetu".
Wa pili ni Steve Jobs aliyefariki mwaka 2009 akiwa na miaka 50. Huyu ni mwanzilishi wa kampuni ya Apple Computers inayotengeneza simu za iPhone, iPads, iMac n.k. Filosofia na mitazamo wa huyu bwana kuhusu maisha na kazi pia umenishawishi kwa kiwango kikubwa katika maisha yangu binafsi. Miongioni mwa mambo ambayo Steve Jobs aliamini na yalinivutia ni pamoja na kuishi kila siku kama ndio siku yako ya mwisho maana ipo siku utakua sahihi.
Steve Jobs aliamini watu ambao ni "wendawazimu" kiasi cha kuamini wanaweza kuibadilisha dunia au kubadilisha jambo fulani katika dunia ndio haswaa huweza kufanya hivyo. Watu wengi wa aina hii katika jamii huonekana kama wendawazimu, wakaidi, wanaojikweza au wasiokubaliana na uhalisia. Alihoji, nini maana ya uhalisia? Aliamini sheria, kanuni na taratibu zilizopo na tunazozifuata ziliwekwa na watu kama mimi na wewe hivyo tukiona hazitunufaishi au kutusaidia kufika malengo yetu tunapaswa kuzibadilisha. Watu wengi huogopa kufanya haya mabadiliko na kulazimika kukubalina na hali ilivyo (status quo) badala ya kuibadilisha kuwa namna wanavyokata. Mwingereza George Bernard Shaw aliwahi kusema “The reasonable man adapts himself to the world; the unreasonable one persists in trying to adapt the world to himself. Therefore all progress depends on the unreasonable man.”
Pia, aliamini namna pekee ya kufanya kazi nzuri ni kupenda kile unachokifanya. Maneno haya nimeyabandika katika ukuta wa sebule yangu kwa zaidi ya miaka saba sasa na ni makusidio yangu mwanangu Lincoln (3) akue akiyasoma. Ukipenda unachokifanya si rahisi kukata tamaa na utafanya kazi kwa kujituma na kwa moyo wako wote.
Aliamini kuwa watu wako radhi kununua bidhaa au kulipia huduma kwa bei yoyote ile utakayo endapo tu hicho kitu au hiyo huduma itaongeza thamani katika maisha yao. Kuna mifano mingi ya hili na yeye alilithibitisha kwa vitendo kwa namna alivyobuni na kuuza bidhaa mbalimbali za Apple ambazo zimeenea na kupendwa duniani kote pamoja na kuwa zinauzwa bei ghali kwa mtu mwenye kipato cha kawaida. Hii fikra kwa kiasi kikubwa imechangia muelekeo wa kibiashara wa kampuni ya BRAINBONGO niliyoanzisha mwaka 2012 nikiwa high-school na marafiki zangu wachache ikiwa na lengo moja kuu; kuwasaidia watu, biashara, makampuni na taasisi kusimulia stori zao kupitia picha bunifu za mnato na nyongefu (creative photography & film) na kwa kupitia ubunifu wa matangazo ya kibiashara kama vile matangazo ya TV, redio, mabango ya barabarani na mitandaoni. Kila mtu ana stori. Kazi yetu ni kukusaidia kuisimulia ya kwako kwa ubunifu na kuifanya kuwa yenye ushawishi. Umeishawahi kujiuliza ni kwa nini unatumia bidhaa au huduma fulani? Vipi kuhusu mwanasiasa uliyempigia kura katika uchaguzi? Kuna msemo unasadikika kusemwa na mwanafilosofia aliyeitwa Plato unaosema, "Those who tell stories rule the world."
Mtu wa tatu na wa mwisho ila sio kwa umuhimu ni mwanamziki na mfanyabiashara wa kimarekani mwenye asili ya Eritrea, Nipsey Hussle. Jina lake kamili ni Airmiess Joseph Asghedom na alizaliwa August 15, 1985 Los Angeles, Marekani na kufariki March 31, 2019 akiwa na miaka 33 pekee kwa kupigwa risasi nje ya duka lake la mavazi linaloitwa The Marathon Clothing. Nipsey anaweza kuwa chaguo la tofauti sana na watu wengine kwenye hii list ila Nipsey ni maana ya halisi ya "Don't judge a book by its cover." Sehemu kubwa ya mwili wa Nipsey uko "covered" na tattoo za kila aina na ukimtazama huwezi kudhani ni mtu wenye upeo mkubwa kifikra na aliyekataa kuruhusu mazingira aliyozaliwa na kukulia kumzuia kuishi maisha ya ndoto zake. Nilimfahamu Nipsey miezi michache tu kabla ya kifo chake na pamoja kuwa kifo chake kilivunja moyo wangu lakini nilikua na nafuu fulani kwamba nilimjua na kurecognize his genius akiwa hai.
Nimefunza mambo mengi sana kutoka kwake ikiwemo uvumilivu na kuwaza long-term katika kufanya maamuzi au kupanga mipango. Nipsey aliwahi kusema, "The highest human act is to inspire". Tafsiri yake kwa Kiswahili ambayo inaweza kuwa haijanyooka sana ni kwamba tendo kubwa zaidi la kibinadamu mtu anaweza kufanya ni kumfanya mtu mwingine aamini inawezekana. Hichi ndicho haswaa kitu Nipsey amekifanya katika maisha yangu. Japokua maisha yetu ni tofauti sana na tumekulia katika mazingira na tamaduni tofauti kabisa ila alithibitisha kuwa chochote kile unachokiazimia kinawezekana ukikipambania bila kukata tamaa. Katika maandiko yajayo nitagusia kidogo kuhusiana na maisha yake na mambo kadha wa kadha aliyoyafanya katika maisha yake binafsi na kwa jamii yake huko Crenshaw, jijini Los Angeles Marekani.
Kutoka kushoto: Samiel (Kaka yake Nipsey), Baba yake, Nipsey Hussle na Adam (mwanzilishi mwenza wa All Money In LLC) |
Nipsey pia aliamini kuwa biashara kama zilivyo mbio za masafa marefu (marathon) na inahitaji uvumilivu mkubwa mwisho. Alizipa bidhaa zake nyingi majina yanayoanzia na neno Marathon kwa sabau aliamini katika mbio za masafa marefu uwezo wa kukimbia umbali mrefu kwa mwendo wa wastani ni muhimu zaidi kuliko kwenda mbio na kuwahi kuchoka wakat umbali bado ni mrefu na vivyo hivyo katika biashara. Katika marathon pia japokua atakaye fika wa kwanza kwenye mstari wa mwisho atatuzwa kama mshindi wa kwanza ila KILA atakaye maliza mbio na kufika kwenye mstari wa mwisho ni mshindi pia, kosa ni tu KUKATA TAMAA. Mara nyingi pia mshindi nambari moja hakuongoza wakati wote wa mbio. Uongozi ni kupokezana. Kuna wakati inabidi upunguze mwendo kidogo kuvuta pumzi, unywe maji na utafute nguvu tena ya kuendelea. Sio ishara ya udhaifu bali ni ishara ya ubinadamu.
Nipsey Hussle akiwa na wanawe Emani na Kross enzi za uhai wake. |
Nipsey pia alisistiza sana katika umiliki wa kazi zake. Na ili uwe mmiliki wa jasho lako ni lazima uwe mzalishaji sio mfanyakazi. Aliamini kama una haki miliki ya kazi yako hususani kazi za sanaa ambazo umiliki wake haushikiki (intellectual property) unajiweka kwenye position nzuri zaidi ya kupata kipato siku za mbele sio tu kipindi umetengeneza. Hii ilidhihirika baada ya kifo chake kilichotikisa ulimwengu wa burudani kwa sababu familia yake iliingiza na inaendelea kuingiza fedha nyingi sana nadhani kuliko hata Nipsey mwenyewe alizoingiza enzi za uhai wake na hii ni kwa sababu alikua anamiliki kazi zake za sanaa kwa asilimia 100% na watu wengi duniani walimfahamu na kuzifuatilia kazi zake baada ya kufariki. Nipsey hadi alipata tuzo 2 za Grammy wakati alishafariki na kuna watu wamefanya mziki miaka nenda rudi, wana majina makubwa na Grammy hawajawahi kupata. Kwa wanaofuatilia sanaa kimataifa wanajua tuzo hizi ndio za heshima zaidi dunia katika maswala ya muziki na ni ndoto ya wanamuziki wengi angalau kupendekezwa kwenye kinyang'anyiro. Hakikisha una miliki kazi yako!
Yapo mengi sana nimejifunza kutoka kwa watu hawa watatu na ni hakika siwezi kuyaelezea yote katika andiko moja na kwa kuwa pia naendelea kujifunza nitaendelea kushare nanyi kadri Mungu atakavyonijalia. Lakini usihadaike, yako mengine mengi ambayo sikukubaliana nayo kutokana misimamo na imani zangu binafsi. "Baba" alishatwambia za kuambiwa changanya na za kwako.
Kwa kuhitimisha, mwandishi maarufu aliyeishi zaidi ya miaka 100 iliyopita aitwae Mark Twain alisema, "Thousands of geniuses live and die undiscovered — either by themselves or by others." Kwa lugha ya kizalendo alimaanisha maelfu ya watu wenye uwezo mkubwa kiakili/kifikra wanaishi na hadi kufa bila kutambulika - wakati mwingine hata wao wanakufa hawajitambui au watu wengine hawawatambui. Naomba nimalize kwa kukuacha na maswali kadhaa; Je, unatambua uwezo wa kipekee ulioko ndani yako? Unafanya nini kuwasaidia wengine wenye uwezo wa kipekee wajitambue au watambuliwe na watu wengine? Au unasubiri mpaka wakifa upost picha ya R.I.P na maneno kedekede ya namna ulivyokua unawahusudu? Majibu unayo mwenyewe ila itakupendaza unaweza kutushirikisha mawazo yako mimi pamoja na wasomaji wengine katika sehemu ya kucomment hapo chini. Ahsante kwa muda wako!
2 Comments
Nice read.
ReplyDeleteThank you for taking the time to read it. Hope it was insightful
DeleteIf you like this post be sure to leave a comment and share it with your friends. It will make my day!